Vijana wameaswa kuwekeza elimu zao katika katika sekta ya kilimo ili kuweza kutatua changamoto ya ajira ambayo imekuwa ni kilio kwa vijana wengi wakitanzania.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa vitabu vilivyoandaliwa na taasisi ya Repoa inayojihusisha na mambo ya utafiti ambavyo vimelenga zaidi kuhusu kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Innocent Bashungwa amesema vijana wanatakiwa wabadilike na wasome alama za nyakati hasa kutokana na mazao yaliyopo hapa nchini yanahitajika katika nchi za jirani ikiwemo Msumbiji, Malawi na mpaka nchi za Ulaya.

“Wakulima wetu wamekuwa wakizalisha mazao bila kujua wanauza wapi lakini ndani ya Serikali hadi sasa mtaona chini ya wizara ya kilimo kuna idara ya masoko kwaajili ya timu ya kutafuta masoko”. Amesema Mh. Bashungwa.

Aidha, Mh. Bashugwa ameongeza kuwa unaweza ukawa kijana si lazima ukashike jembe unaweza ukaanzisha kampuni ambayo imejikita katika masoko ya mazao ya wakulima wa hapa nchini na ikawa ajira kwako.

Katika vitabu ambavyo vimezinduliwa na Mh. Naibu Waziri vimelenga kutoa elimu juu ya kilimo pamoja na umwagiliaji hasa kutokana na tafiti ambazo walizifanya Repoa.