Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa anaiwekea vikwazo vikali Iran ikiwemo afisi ya kioingozi mkuu wa dini Ali Khamenei

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Bwana Trump amesema kuwa vikwazo hivyo vya ziada ni kujibu hatua ya Iran kuiangusha ndege isio na rubani ya Marekani na mambo ‘mengine mengi’.

Ayatollah Khamenei , ambaye ndio kiongozi mkuu nchini Iran alilengwa kwa kuwa ndiye anayehusika na hali ya uhasama katika utawala wa taifa hilo.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini humo Mohamed Javd Zarif alisema kuwa Marekani haipendelei diplomasia.

Katika ujumbe wa Twitter kufuatia tangazo la rais Trump, bwana Zarif pia aliushutumu utawala wa Trump kwa kuwa na kiu ya vita

Hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili imekuwa ikipanda katika wiki za hivi karibuni.

Hatahivyo waziri wa fedha nchini Marekani Steve Mnuchin alisema kuwa maagizo ya rais Trump ambayo yatazuia mabilioni ya madola ya mali ya Iran yalikuwa yanaandaliwa hata kabla ya Iran kuiangusha ndege ya Marekani isiokuwa na rubani katika Ghuba wiki iliopita.

Wizara ya fedha nchini Marekani imesema kuwa makomanda wanane wa Iran ambao husimamia kitengo kinachoshauri vitendo vya jeshi kuu la {Islamic Revolution Guard Corps} IRGC walikuwa wanalengwa katika vikwazo hivyo vipya.

Iliongezea kuwa agizo la rais Trump pia litaunyima uongozi wa Iran kupata raslimali za kifedha mbali na kuwalenga watu walioajiriwa na kiongozi huyo wa dini katika afisi kadhaa ama nyadhfa tofauti mbali na taasisi za kigeni za kifedha ambazo huwasaidia kufanya biashara.

Marekani imedai kwamba Ayatollah Khamenei ana utajiri mkubwa ambao unafadhili jeshi la IRGC.

Mwaka 2018 waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Mike Pompeo alisema kwamba kiongozi huyo ana utajiri wenye thamani ya $95b ambao hutumika kulifadhili jeshi hilo.

Vikwazo pia vitamlenga waziri wa maswala ya kigeni bwana Javad Zarif baadaye wiki hiki , kulingana na bwana Mnuchin.

Mnamo mwezi Mei 2018, Ikulu ya Whitehouse ilirejesha vikwazo vyote ambavyo vilikuwa vimeondolewa dhidi ya Iran chini ya mkataba wa kinyuklia wa Iran ambao uliafikiwa na viongozi wa mataifa yenye uwezo mkubwa duniani ili kuizuia Iran kutengeza silaha zake za Kinyuklia.

Vikosi vya Marekani Ghuba

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili uliharibika mnamo mwezi Mei -mwaka mmoja baada ya bwana Trump kujiondoa katika mkataba huo wa Kinyuklia , Marekani ilianzisha shinikizo dhidi ya Iran kwa kuziondolea ruzuku nchi ambazo zinanunua mafuta kutoka Iran.

Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulizi dhidi ya meli za mafuta katika Ghuba , ambayo Ikulu ya Whitehouse inasema kuwa Iran ndio ya kulaumiwa.

Tehran hatahivyo imekana madai hayo. Baadaye Maafisa wa Iran walisema kuwa taifa hilo litakiuka dhidi ya kiwango cha uzalishaji wa madini ya uranium yanayotumika kutengenezea silaha za kinyuklia.

Siku chache baadaye , ndege ya Marekani isiokuwa na rubani ilishambuliwa na majeshi ya Iran na kuangushwa katika kile ambacho Marekani inasema ni maji ya kimataifa , lakini Iran inasema kuwa ndege hiyo ilikuwa katika himaya yake.