Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya upande wa serikali kumaliza kutoa ushahidi.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa CHADEMA,  Freeman Mbowe, mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa-Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Ikumbukwe washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.