Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Liberatus Sabas amebainisha kuwa wanaendelea na msako wa kumnasa mwanaume aliyeonekana kwenye mitandao ya kijamii akiwa na msanii Wema Sepetu, katika video iliyokuwa na maudhui ya kingono ili kumfikisha mahakamani, kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Watu wanadhani labda jeshi la polisi limeshaachana na mwanaume huyo lakini bado ni mtuhumiwa na hivyo akikamatwa anapelekwa mahakamani, polisi tunaendelea kumtafuta huyu jamaa, hatujakata tamaa”, amesema Kamanda Sabas.

Mwezi uliopita kupitia mitandao ya kijamii, zilisambaa video za mwanadada Wema Sepetu akiwa na mwanaume aliyedai kuwa ni mume wake mtarajiwa ambaye alimpost siku za hivi karibuni katika ukurasa wake wa instagram.

Baada ya kusambaa kwa video hiyo yenye maudhui ya ngono mwanadada huyo aliomba radhi kwa mashabiki wake, na kudai kuwa amebadilika na hatorudia tena maisha yake ya awali lakini kauli hiyo haikubadili mtazamo na sheria za makosa ya mtandaoni.

Ambapo kufuatia kosa hilo Novemba mosi Wema alipandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu ambapo alikana mashtaka ya kusambaza video hizo na kuachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 na kutakiwa kutochapisha picha wala maneno yanayoashiria maudhui yoyote ya kingono.