Vituo 13 vya radio na Televisheni nchini Uganda vimefungiwa kwa pamoja na kufutwa kazi baadhi ya wanahabari kwa ”kupotoshaji’ na kuchochea ghasia kwa kutangaza taarifa zilizo na “ujumbe na hisia kali”.

Tume ya mawasiliano ya nchini Uganda imesema kuwa vyombo hivyo vya habari vilikiuka kanuni ya kifungo cha 31 ibara ya 4 ya sheria ya mawasiliano ya Uganda ya mwaka 2013.

Chama cha wanahabari nchini Uganda (UJA) kimeelezea kughadhabishwa na hatua hiyo.

”Wanahabari karibu 30 wanakabiliwa na tishio la kufutwa kazi na hili litakuwa na athiri kwa taalumu zao tu bali mamilioniya waganda watakosa huduma ya kupashwa habari” alisema taarifa ya chama hicho.

UJA pia iliongeza kuwa serikali kupitia mashirika yake ya udhibiti wa mawasiliano inatakiwa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Kuna madai kuwa huenda hiyo imetokana na mtangazo ya moja kwa moja ya kukamatwa na kushtakiwa kwa mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Kyagulanyi kwa sasa anazuiliwa rumande na anatarajiwa kufikishwa tena mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Buganda Road leo Alhamisi.

Tume hiyo imedai kuwa iliwahi kutoa onyo kuhusiana na suala hilo lakini baadhi ya vyombo vya habari havikutilia maanani onyo hilo.