Vodacom yaja na Tecnolojia ya kununua Apps kutoka Google Play Store bila ya kutumia (Credit Card)

Kwa sasa wapenzi wa kununua programu za simu (Apps) kutoka katika duka la Google Play Store hawatapata tabu tena ya kufanya malipo baada ya mtandao wa simu za mkononi wa Vodacom Tanzania kuzindua huduma ya kulipia kwa njia ya vocha (muda wa maongezi).

Mfumo huu utasaidia mteja kufanya manunuzi ya Apps kwa njia ya simu za mkononi, bila kulazimika kutumia malipo ya benki ambayo yana mchakato mrefu kidogo na muda mwingine sio salama katika ulinzi wa akaunti yako.

Hatua hiyo, imekuja baada ya Mtandao pendwa wa simu za mkononi nchini Tanzania wa Vodacom, kuingia makubaliano ya kibiashara na kampuni ya Google ambayo inamiliki duka la mtandaoni la ‘Play Store’.

Kuanzia sasa wateja wenye vifaa au simu za ‘Android‘ ambao walikuwa wanatumia huduma za kibenki katika kununua programu mbalimbali za simu kupitia Google Play Store, wataweza kununua Apps kwa kutumia simu zao moja kwa moja.

Hatua hiyo iliyopigwa na Vodacom ni miongoni mwa mikakati ya kuboresha na kuimarisha mfumo jumuishi wa kifedha ambao unaziunganisha taasisi za fedha na watoa huduma mbalimbali duniani na kuondokana mfumo wa zamani wa kubeba fedha mfukoni au kwenda benki moja kwa moja.