Vyombo vya habari vyatakiwa kusitisha kupiga muziki wa Burudani katika kipindi hiki cha maombolezo

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, inaendelea kuvisisitiza vyombo vya habari vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii, kutii agizo la kusita kupiga aina yoyote ya muziki wa burudani.

Taarifa iliyotolewa Mrajis wa Tume ya Utangazaji Omar Said Ameir, imesema kutokana na msiba mkubwa uliolikumba taifa kwa kuzama  kivuko cha MV Nyerere katika Ziwa Victoria juzi, vyombo vya habari vinapaswa kuheshimu agizo la serikali kuungana na Watanzania waliopoteza ndugu zao kwenye ajali hiyo.

Ameir amefahamisha kuwa, nyimbo zinazoruhusiwa kupigwa katika kipindi hiki cha maombolezo kitaifa, ni zile zinazoelezea huzuni na matukio ya misiba katika kuzifariji familia na wananchi wote walioguswa na janga hilo.

Aidha, alieleza kuwa kasida zenye maudhui ya majonzi pamoja na nyimbo za kwaya au za dansi zinazoelezea dhana ya kifo na misiba, ndizo zinazopaswa kupea nafasi kwa sasa.

Kutokana na tukio hilo, tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, imetangaza siku nne za maombolezo zilizoanzia Ijumaa ya Septemba 21, 2018 hadi saa 6:00 usiku wa Jumatatu Septemba 24.

Katika kipindi hicho, bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Kivuko cha MV Nyerere kinachofanya safari katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza, kilipinduka na kuzama mchana wa Septemba 20 ambapo zaidi ya watu 136 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.