Waandishi wa habari wametakiwa kuwa weledi wa kufichua habari  hususan habari zinazohusiana na watoto katika suala zima la udhalilishaji ili kuiokoa jamii na kilio hicho.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar. Riziki Pembe Juma wakati akifungua mafunzo ya wakufunzi wa waandishi wa mradi wa utetezi wa haki za watoto ulioandaliwa na Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) kwa kushirikiana na Shirika la umoja wa Mataifa linaloshuulikia watoto (UNISEF) huko Chuo cha Waandishi wa Habari kilimani Wilaya ya Mjini Unguja.

Akieleza kuhusu taarifa za utafiti zilizofanywa na UNISEF amesema kuwa udhalilishaji wa watoto walio na umri wa miaka miwili unaongezeka kwa kasi kwani kiasi cha watoto bilioni moja wanaodhalilishwa Duniani ni kati ya miaka miwili hadi kumi na saba na kwaupande wa Zanzibar hali hii inasikitisha kwani vitendo vingi vya udhdlilishaji wa watoto vinafanywa na watu wa karibu na familia wakiwemo na marafiki na ndio maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashirikiana na wadau wa mashirika ya kimataifa na Taifa ili kupambana na tatizo hilo.

Nae Mwenyekiti kutoka Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar WAHAMAZA Salim Said Salim amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwalengo la kuwajengea uelewa wanahabari pasipo na usumbufu wowote ili kutambua kwa undani haki ambazo zinazostahiki kupatiwa kwa mtoto na wakufunzi hao wanapotoa habari zao ziwe na usawa.

Nae Afsa Uhusiano kutoka UNISEF  Usia Ledama amewataka wakufunzi wanaopewa mafunzo hayo kuwa na uelewa wa kufuatilia mikakati dhidi ya vitendo vya kikatili kwa watoto ili kulisaidia Taifa kwani watoto ndio nguzo ya baadae.

Mafunzo hayo yamefunguliwa leo  Juni 10 – 2019 na yanatarajiwa kumaliza Juni 12 -2019