Wabunge wanawake waanza kutekeleza agizo la Ndugai

Agizo la Spika wa bunge Job Ndugai kwa wabunge wanawake kutobandika kucha na kope za bandia wanapoingia bungeni, limeanza kutekelezwa.

Mwanzoni mwa wiki Spika Ndugai alipiga marufuku kwa wabunge wanawake wanaobandika kucha na kope za bandia wasiingie bungeni na siku moja baadaye wabunge wanawake waligawanyika kuhusu kauli hiyo baadhi wakisema kuwa anaingilia uhuru wa watu.

Jana wabunge wanawake ambao mara kadhaa walionekana kuwa na kope na kucha bandia  hawakuwa nazo. Hata hivyo hakukuwa na ukaguzi wowote kwa wabunge wanawake katika lango la kuingilia.

Wabunge wengi hasa vijana, walionekana bila kucha wala kope licha ya kuwa lilikuwa ni zoezi gumu kuwabaini waliobandika kucha.

Jana Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai alisema kuwa kauli ya spika haikuwa ya utani kwani alizungumza akiwa kwenye kiti hivyo isingekuwa ni utani.

Hata hivyo alikataa kuzungumza kwa undani namna ukaguzi utakavyokuwa ukifanyika kwa wabunge kabla ya kuingia ndani na iwapo mbunge atabainika ni adhabu gani zinaweza kuchukuliwa.

Jambo hilo pia linaweza kuleta ukakasi kwa wageni wanaotembelea bunge kwani mara nyingi wageni hutakiwa kuakisi mavazi na mienendo ya wabunge hivyo zoezi la kuwazuia wabunge kutokuwa na kote na kucha bandia, linaweza kuwaathiri na wao pia.