Zakayo Muyunga na Ayoub Mpimbi wakazi wa Izumbi ambao ni Wachimbaji wa Dhahabu katika kijiji cha Izumbi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika Mgodi wa Mwembe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ulrich Matei amesema, tukio hilo limetokea siku ya Julai 2, 2019 majira ya saa 10 jioni”Wakati wanafanya shughuli hizo basi waliangukiwa na kifusi cha udongo mchanganyiko na mawe na kusababisha kifo chao baada ya kukosa hewa. Mwamba huo unamilikiwa na mtu mmoja anayejulikana kwa jina la  Mwembe Msemakweli, na sisi kama jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hizo, tulifika eneo la tukio na kuthibitisha na marehemu walifariki wakati wanakimbizwa Zahanati”, amesema Kamanda Matei.

Kamanda Matei ametoa rai kwa wale wanaofanya shughuli za uchimbaji, akiwataka kuwa makini wakati wa kufanya shughuli zao, na kwamba  shughuli ya kupanga mbao za kuzuia vifusi waifanye kabla hawajaingia ndani ya shimo badala ya kupanga wakiwa ndani ya shimo.