Baraza la Manispaa la Mjini Magharibi Unguja linaendelea na harakati zake za kukagua usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Mji na kuhakikisha unakuwa safi.

  Hatua hiyo imekuja baada Ya kuona hali ya usafi katika mji wa Zanzibar inapungua kwa baadhi Ya maeneo watu hufanya uchafu katika maeneo yao wanayoishi pamoja na sehemu za kuuzia vyakula (Vioksi) na maeneo yenye bucha za Nyama.

Akizungumza na Zanzibar24 huko ofisin kwake Malindi Mjini Zanzibar Afisa Uhusiano wa Baraza la Manispaa la Mjini Magharibi Hassan Yahya Hassan amesema lengo la kukagua sehemu hizo ni kuhakikisha watu wanadumisha usafi katika maeneo Yao ikiwemo sehemu zao za kufanyia biashara na nyenginezo.

Amesema zoezi hilo limeanza tangu wiki iliyopita Ya tarehe 30 October ambapo wanafanya zoezi la kukagua maeneo yasiyo safi yanayoharibu mandhari Ya Mji wa Zanzibar .

Aidha Hassan amesema wafanyabiashara wanaogundulika na makosa tofauti ya kimazingira huwatia hatiani na kuwapeleka mahakama Ya mwanzo Malindi kwa ajili Ya kuwachukulia hatua Za kisheria.

Amesema jumla ya wafanyabiashara 9 wamekamatwa kutokana na kueka mazingira machafu pamoja na kutokuvaa sare za kazi ambapo  kwa wamiliki wa Mabucha waliokamatwa watatozwa kila mmoja Tsh. 25,000/= na wenye Vioksi vya vyakula Tsh. 50,000/=.

Sambamba na hayo Hassan ametoa wito kwa jamii kuhakikisha wanafata maelekezo yote yaliyotolewa na wizara Ya afya pamoja na miongozo ya baraza la manispaa ili kuhakikisha wanafanya biashara zao sehemu safi bila kuhatarisha maisha Ya watumiaji.

Na Rauhiya Mussa Shaaban