Mkuu wa wilaya ya kaskazin B Aboud Hassan Mwinyi amewataka wafanyakazi wa Hoteli mbalimbali  walioachishwa kazi kwa ugonjwa wa corona kuwa wastaamilivu wakati uongozi wa wilaya unalitafutia ufumbuzi tatizo la  fedha zao kutoka mfuko wa hifadhi ya jamii zssf

Akizungumza na wananchi wa shehiya za Mahonda na mkataleni akiwa na kamati ya ulinzi na usalama na watendaji mbalimbali wa serikali katika mkutano maalumu wa kusikiliza matatizo ya wananchi amesema ili kumaliza tatizo hilo upo muhimu wa kupata muongozo wa kisheria kwa wafanyakazi waliosimamishwa kazi kama wana uhalali wa kulipwa fedha hizo kwa sasa

Amefahamisha kuwa lengo la fedha za zssf ni kwa ajili ya malipo ya mfanyakazi baada ya kustaafu hivyo ikiwa hakutakuwa na uhalali wa kulipwa fedha hizo uongozi wa wilaya utatafuta njia mbadala ili kuweza kuwasaidia wafanyakazi hao

Akizungumzia  tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji Aboud amesema serikali ya wilaya inakusudia kujenga mji kwa kutenga  maeneo maalumu kwa ajili ya ufugaji ,kilimo,soko pamoja na maeneo kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwemo afya ili kumaliza matatizo hayo

Injinia kutoka shirika la umeme mkoa wa kaskazin Unguja Yussuf Hamadi Omari amesema tatizo la umeme mdogo katika eneo la mahonda litashughulikiwa kwa kuweka transfoma mbili kubwa pamoja na wananchi kuwa wastaamilivu kuhusu bei ya kuunga umeme kwani shirika  linaangalia uwezekano wa kupumguza bei huyo.

Kwa upande wao wananchi baadhi ya wananchi wamemuelezea mkuu huyo wa wilaya kuwa katika shehiya zao wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ubovu wa barabara za ndani,madai ya fidia ya barabara kutoka kwanyanya  hadi mkokotoni,wizi wa mazao, ukosefu wa maji pamoja na malipo madogo ya wafanyakazi wa mashamba ya kiwanda cha sukari mahonda.