RAIS  wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi amewasamehe  wafungwa 700 wa kisiasa waliofungwa jela na utawala wa mtangulizi wake, Joseph Kabila.

Tshisekedi alisaini amri ya rais ya kuwasamehe wafungwa hao  na kutimiza ahadi aliyoitoa mwanzoni mwa mwezi huu, kwamba hilo ni moja kati ya mambo atakayoyafanya katika siku zake 100 za kwanza madarakani.

Miongoni mwa walioachiwa huru ni Firmin Yangambi, aliyehukumiwa mwaka 2009 kifungo cha miaka 20 gerezani kwa makosa ya kutishia usalama wa taifa.

Mwanasiasa mwingine aliyeachiwa huru ni Frank Diongo kiongozi wa upinzani aliyehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.

Tshisekedi alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Desemba 30 mwaka ulioputa ambapo Congo ilishuhudia ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani, ikiwa ni mara ya kwanza tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka Ubelgiji karibu miaka 60 iliyopita.

Chanzo Zanzibar leo