Wafungwa wateka gereza Sudan Kusini

Mamlaka nchini Sudan Kusini inaendelea na mazungumzo dhidi ya wafungwa ambao wamejihami kwa bunduki na visu, na ambao wanashikilia eneo la gereza hilo mjini Juba wakishinikiza kuachiwa huru kwa wafungwa wa kisiasa kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Rais Salva Kiir.

Wafungwa hao walifanikiwa kuchukua Bunduki na visu kutoka ndani ya ghala la kuhifadhia silaha.

Vikosi vya usalama vimelizingira gereza hilo ambalo pia ni makao makuu ya shughuli za wa taifa.

Awali Rais Salva Kiir alitoa ahadi kwamba angeliwaachia wafungwa wa kisiasa wanaoshikiliwa nchini humo jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.

Hata hivyo msemaji wa Polisi ametupilia mbali madai hayo na kuongeza kuwa kulikuwa na wafungwa 400 katika gereza hilo,na kwamba wafungwa wapatao 60 ndiyo walioanzisha vurugu na mgomo.

Inadaiwa kuwa wafungwa hao walimzidi nguvu mlinzi wa gereza hilo katika eneo la lango la kuingilia na kisha wakavunja milango kwa risasi.

Mara kadhaa wafungwa nchini Sudan Kusini wamekuwa wakilalamikia hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa madai kuwa wanashikiliwa kinyume cha sheria.

Taifa hili la Sudan Kusini lenye idadi kubwa ya vijana, mwaka 2011 lilijitenga na Sudan ya Khartoum baada ya kuwa na harakati za muda mrefu za kusaka uhuru wake.

Lakini miaka miwili tu baadaye mgogoro mpya ulizuka baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu kiongozi wa waasi Riek Machar kwamba alikuwa akifanya mipango ya mapinduzi.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilisababisha vifo vya watu takriban 380,000,idadi kubwa ya watu kufa kutokana na machafuko.