MUFTI Mkuu wa Zanzibar, Shekh Saleh Omar Kaabi, amewataka waumini wa dini ya kiislamu kutumia nyumba ya ibada ili kujipatia elimu.

Aliyasema hayo katika ufunguzi wa mskiti wa Jambiani Wilaya ya Kusini Unguja, uliojengwa na Taasisi Muzdalifa chini ya ufadhili wa Taasisi ya Al-Ansari Foundation kutoka nchini Uengereza.

Akimuwakilisha Mufti Mkuu wa Zanzibar, Kadhi  wa Wilaya Mjini Unguja, Shekh Othman Ame Chum, alisema iwapo waumini hao watakuwa na mashirikiano ya pamoja wataweza kuendeleza ili  kuleta maendeleo kijijini hapo.

“Wakitumia vyema msikiti huu kwa pamoja wataweza kujenga mustakbal mzima katika kuendeleza kwa faida ya sasa na baadae” alisema.

Alisema  msikiti  ni moja ya sehemu ama taasisi ya kuweza kukaa waumini kwa pamoja bila ya kuangalia tofauti zao za rangi, kielimu, kihali na badala yake kukaa na kujadili mambo yanayohusu ya kimaisha.

Hata hivyo amewasisitiza wananchi wa kijiji hicho kuendelea kusali, ili kuleta baraka za Mtume Muhammada S.A W. na kupata fadhila zake na amewasihi wananchi hao kuendelea na kuimarisha mskiti huo, ili kufanya ibada ya sala pamoja na kutumia shughuli zao za kila siku.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatahamini michango inayotolewa na taasisi binafsi kwa kuwasaidia wananchi na serikali kwa kutataua changamoto mbali mbali za kijamii ikiwemo elimu ya Akhera.

Akizungumza suala la udhalilishaji kadhi huyo alisema hivi sasa kumekuwa na matatizo ya udhalilishaji kwa watoto hivyo ni vyema wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao katika kufatilia mienendo yao, ili kuwaepusha na vitendo hivyo.

Aidha alisema kumekuwa na changamoto ya mitandao ya kijamii ambayo inawapotosha watoto hivyo ni vyema kila mmoja amwe mchunga na kuwataka wazazi kuwa na malezi ya pamoja na kuwaomba wafadhili hao kuendelea kusaidia kujenga Ukuta ili kuepusha na wizi.

Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Muzdalifa, Shekh Abdalla Ghadhal Abdalla kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Muzdalifa Shekh, Farouk Hamad Khamis, alisema Taasisi yake imekuwa na kawaida ya kujenga misikiti, kuchimba visima maeneo mbali mbali na masuala mengine kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa wa vijijini.

Hivyo amewapongeza wafadhili kwa kuwajali kuwasaidia na kuwataka wasimamizi kuutumia vizuri mskiti  na kisima ili kuweza kuwanufaisha vizazi vya sasa na vya baadae.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Al-Ansari kutoka nchini Ujerumani Javed Ansari alisema wataendelea kuisaidia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuunga mkono wananchi wake kwa  kuwapatia mambo mbali mbali ikiwemo ujenzi wa  miskiti, madrasa na kuchimba visima ili kuondokana na matataizo yanayo wakabili.