Wananchi wa Kijiji cha Binguni Wilaya ya Kati Unguja wameomba kushirikishwa kikamilifu katika Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Binguni ili kupata fursa mabalimbali ikiwemo ajira kwalengo la kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza.

Wamesema hayo wakati wakitoa wasiwasi wao baada ya kuona ujenzi huo umeshaanza kwa baadhi ya vitengo kujengwa katika eneo hilo na bado hakuna mwanakijiji aliyechukuliwa na kushiriki harakati za ujenzi huo ambae anatokea katika kijiji hicho.

Wamesema katika Kijiji chao vijana wengi hawana ajira maalum na kupelekea kukaa vijiweni bila ya kujishughulisha na chochote jambo ambalo linapekekea hali ngumu ya maisha na kukosa muelekeo.

Wamefahamisha kuwa mara baada ya kuona harakati za ujenzi umeshaanza wamepata faraja kubwa na kutarajia kupata ajira kutokana na fursa hiyo kuja katika kijiji chao lakini bado katika hatua za awali harakati za ujenzi huo umeshirikisha watu wasiowafahamu jambao ambalo limewatia wasiwasi.

Aidha wameeleza kuwa kwa baadhi ya maeneo endapo itatokea fursa kama hiyo vijana na wakaazi husika ndio wa mwanzo kushirikishwa hivyo uongozi wa Shehia ya Binguni nao wanahaki ya kuwashirikisha ipasavyo kwa lengo la kujisaidia kiajira.

 Walifafanua kuwa Mradi wowote wa maendeleo kikawaida hushirikishwa na wakaazi wa maeneo husika kwa kupata nafasi ya kushirikishwa kwa baadhi ya mambo ikiwemo vibarua.

“Kweli watu wa huku hatukusoma basi hata vibarua wa kubeba zege ambalo halihitaji hata kusoma haitakuwa vyema tukinawaona watu ambao hatuwajui wanashiriki harakati za kubeba zege na mambo mengine” walisema wakaazi hao.

Wamesisitiza kuwa ukosefu wa ajira ni tatizo linaloikabili Nchi nyingi Duniani hivyo zikikitokea fursa ndogondogo katika jamii hapana budi kushirikishwa angalau kwa baadhi ya vijana ambao wanaweza kufanyakazi.

Nae Sheha wa Shehia hiyo Ali Yussuf Mussa amesema kuwa maandalizi na ujenzi wa baadhi ya taasisi za Hospitali hiyo unajengwa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na haukushirikisha wananchi wa kawaida kwa sasa.

 Amefahamisha kuwa kwa sasa ujenzi huo umesimama na wakati wowote kampuni kutoka China itakuja kuendelea na ujenzi huo ambapo wanatarajia kuchukua wakaazi wa maeneo husika endapo watahitaji wafanyakazi wengine.

Aidha amefahamisha kuwa baadhi ya wananchi wanatabia ya kudharau mambo kwani wanapoitwa vikaoni kwa ajili ya kupatiwa taarifa fulani hawashiriki ipasavyo jambo ambalo linawakosesha fursa kutokana na baadhi yao kukosa taarifa hizo.

Hata hivyo Sheha Yussuf amewataka wananchi hao kuhudhuria na kushiriki kwa wingi vikaoni pindi wanapohitajika kufika ili kuondosha malalamiko yanayoweza kujitokeza.