Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili Judith Amoni Mwansansu(39) na Aive Alex Swalo(17) kwa kosa la kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto, Daines Kefas Mwansasu(06) vya kumuunguza kwa moto na kumpiga.

Kamanda SACP Ulrich Matei, amesema tukio hilo lilifanyika Jumanne July 31, 2018 majira ya saa tatu usiku ambapo siku iliyofuata Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa raia wema kwamba mtoto huyo amejeruhiwa sehemu mbalimbali kwa moto.

Inadaiwa siku hiyo ya Jumanne, Daines alikuwa ameenda kucheza na rafiki zake na aliporudi nyumbani majira ya jioni shangazi yake alimuadhibu kwa kumchapa na waya wa umeme sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha na maumivu makali mwilini.

Aidha, August 1, 2018 majira ya asubuhi, watuhumiwa (Shangazi akishirikiana na Mwanae) waliendelea kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto huyo kwa kumuunguza kwa moto sehemu za miguuni na kwenye makalio.

Watuhumiwa wote wawili wamekamatwa kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo huku Daines akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.