Viongozi wa Skuli za Wilaya ya Magharibi B Unguja wametakiwa kuwasimamia Walimu kusomesha kwa kufuata Misingi na Maadili ya fani yao ili kuepuka Migogoro inayoweza kuepukika.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi B Ali Abdallah Natepe katika hafla ya kuwaaga Waalimu waliostafu na kuwapongeza Wanafunzi waliofaulu Michipuo katika Skuli ya Msingi Kiembesamaki.

Amesema iwapo watasimamia kwa nguvu moja kutapelekea kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi wao.

Amefahamisha kuwa lengo la Serikali kuweka madaraka mikoani ni kuhakikisha inatoa huduma kwa urahisi kwa Wananchi ili kuwaondoshea usumbufu wanaoupata Waalimu katika Skuli zao na kuwawezesha Wanafunzi kusoma katika Mazingira mazuri bila usumbufu wowote.

Amesema mivutano katika Skuli haileti maendeleo yoyote katika sekta ya Elimu hivyo ni vyema kuiepuka na kufanya kazi kwa kufuata Misingi ya Sheria za nchi na kufikia Azma ya Serikali ya kutoa elimu kwa wote.

Kwa upande wake Afisa Elimu Wilaya ya Magharibi B Soud Hassan Soud amesema Manispaa imeweka Mikakati Madhubuti ya kuwawezesha Walimu kusomesha kwa bidii ili wanafunzi wao waweze kufaulu vizuri Mitihani ya Taifa.

Aidha amewaomba Walimu hao kuunga Mkono mikakati hiyo iliowekwa na Baraza hilo ili kuhakikisha wanasomesha katika mazingira bora itakayopelekea kufanya vizuri watoto wao.