Walimu mikononi mwa Polisi kwa kumshambulia mwanafunzi hadi kuzirai

Walimu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi wa kike kidato cha tano hadi kuzirai kwa madai ya kutoga masikio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mpojoli Mwaburambo, alithibitisha jana kuwapo kwa tukio hilo. Alisema mwanafunzi huyo Anneth Kulwa (19), baada ya kushambuliwa alikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ambako alitibiwa na kupatiwa fomu Na. 3 ya Jeshi la Polisi (PF3).

Kamanda Mwaburambo alisema tukio hilo lilitokea Desemba 12, majira ya saa 5 asubuhi katika Shule ya Sekondari Kasamwa, Wilaya ya Geita, mkoani Geita, na chanzo kinadaiwa kuwa walimu hao kumtuhumu mwanafunzi huyo na wenzake saba kutoga masikio na kuchukua jukumu la kuwaadhibu.

Alisema baada ya tukio hilo kubainika, polisi ilifuatilia kwa kuchukua maelezo ya wanafunzi na kufunguliwa jalada la uchunguzi. Aidha, Kamanda alisema polisi walifika eneo la tukio na kuwakamata watuhumiwa na kuahidi kuwa uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Akizungumzia tukio hilo akiwa wodini, mwanafunzi huyo alisema anakumbuka kabla ya kupoteza fahamu yeye na wanafunzi wenzake saba walikuwa wakishambuliwa na walimu kwa kipigo cha viboko, makofi na mateke.

Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kasamwa, Happy Magati, alikiri kutokea tukio hilo, lakini akadai asingeweza kulizungumzia kwa kina kwa sababu tayari lilikuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa uchunguzi.