Walimu na wazazi wa Wilaya ya Kaskazini A wakiwa katika mafunzo maalum yaliyofanyika Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A wametakiwa kushirikiana katika kudhibiti nidhamu maskulini na kukabiliana na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na wanafunzi ikiwemo utoro.

Akisisitiza masuala hayo Mkurugenzi  Idara ya Elimu Maandalizi  na Msingi Safia Ali Rijali amewataka walimu wakuu,wazazi na kamati za Skuli  kushirikiana kudhibiti tatizo la  utoro ,udhalilishaji,mimba na ndoa za umri mdogo   ili kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya Elimu.

“mimba za umri mdogo ndoa za mapema na utoro mashuleni ndio chanzo kikuu kinachorejesha nyuma maendeleo ya Elimu kwa watoto”alisema Bi Safia.

Aidha Bi Safia alisema kuwa ukosefu wa elimu kwa mtoto kunapelekea kukosekana kwa wataalamu mbali mbali nchini,sambamba na ongezeko la vitendo viovu ikiwemo udhalilishaji.