WANAWAKE mkoani Tabora wamekuwa wakitumia tumbaku  na ugoro ambayo huiweka sehemu za siri ili kupunguza hamu ya tendo la ndoa.

Kwa mujibu wa uchunguzina mahojiano yaliyofanywa na shirika la habari la Uingereza (BBC), tabia hiyo imezoeleka sana miongoni mwa wanawake wasio na wenza wao, wakiwemo wajane. Hata hivyo, kitendo hicho kinasemekana huwa hakina madhara kwa afya zao.

Wanawake, hususan wasio kuwa katika uhusiano na wanaume ama kuolewa, hutumia njia mbalimbali kumaliza hamu zao.

”Mimi ni mjane, natumia tumbaku katika kumaliza hamu zangu kwa sababu sina mwanaume na wala sitaki mwanaume mwingine.  Kwa wiki naweka mara mbili,” anasema Zaituni Shaban,  mmoja ya wanawake wanaotumia tumbaku kwa kuziweka sehemu za siri.

Mwanawake mwingine, Asha (si jina lake halisi) amesema anatumia tumbaku kwa sababu alikimbiwa na mwanaume wakati ana ujauzito.

”Kwa kweli sitaki kusikia tena wanaume, mi nitabaki na tumbaku, maana nikitumia hamu yote inaisha sina haja tena,” anasema.

Wanawake wote waliozungumza wanakiri kuwa matumizi ya tumbaku sehemu za siri huwasaidia kumaliza hamu ya tendo la ndoa.

Kwa mujibu wa wanawake hao,  huchukua majani makavu ya tumbaku kisha kuyatangwa na baada ya hapo huchanganya na mafuta kidogo pamoja na magadi, na mara nyingine hutumia ugoro kufanya mchangayiko huo. Baada ya hapo huweka sehemu za siri na kisha hupata mwasho ambao  humaliza haja ya tendo la ndoa.

”Mi  huwa napaka mara mbili kwa wiki na huwa naweka kwa muda kidogo kabla ya kuondoa na kisha napata mwasho, na wala sipati maumivu yoyote nikimaliza matamanio yangu ya kufanya tendo la ndoa mambo yanakuwa yameisha,” anasema Zaituni.

Kwa kawaida wanawake hawa baada ya kupaka tumbaku ama ugoro sehemu za siri husikia kama wamekutana kimwili na wanaume.

Katika kijiji cha Ugala, suala hili ni jambo la kawaida miongoni mwa wanawake lakini kwa upande wa wanaume si wengi wanalijua  na wanaojua wanasema kuwa imekuwa siri baina ya wanawake tu.

“Mimi nimekuwa nikisia lakini mara nyingi  kwa bahati mbaya wakiongea na nikuwauliza, wanasema ni siri yao baina ya wanawake na si wanaume,”anasema anasema mzee Usantu mmoja wa wakazi wa kijiji hicho cha Ugala.

Kwa mujibu wa baadhi ya wanawake wanaotumia tumbaku sehemu zao za siri, wanasema hawajawahi kupata tatizo lolote kiafya.

Lakini mtaalamu wa magonjwa ya kinamama anasema kuwa baadhi ya wanawake wanaokutwa na viashiria vya saratani hasa ya kizazi wamekuwa na historia ya kutumia tumbaku sehemu za siri.

“Hatuna utafiti wa moja kwa moja lakini data za kwetu hapa wakati tunawahoji tabia za mazoea walizonazo,  baadhi wamekiri kutumia tumbaku, hivyo hiyo inaweza kuwa miongoni mwa sababu, ” anasema daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Matumizi haya ya tumbaku kwa asilimia kubwa yamechangiwa na uelewa mdogo wa wanawake wa kijiji hicho juu ya madhara ya kiafya wanayoweza kupata.

CHANZO: BBC SWAHILI