Wanafunzi nchini wametakiwa kuzitumia Serikali za wanafunzi Zilizoanzishwa mashuleni kuelezea matatizo yanayowakabili ili yapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Hayo yameelezwa na Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Kiislamu ya Mluka bin Alawiy Aisha Abdallah Alawiy mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Raisi wa Skuli hiyo iliopo Kiponda Wilaya Mjini.

Amesema Wanafunzi wengi wanapopata matatizo wanashindwa kuyapeleka moja kwa moja kwa uongozi hivyo ni vyema kuitumia serikali hiyo kupeleka malalamiko yao na kufikishwa sehemu husika.

Aidha amesema serikali hizo zinatoa fursa ya wanafunzi kuweza kujifunza masuala ya uongozi mapema,kupiga vita utoro na kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri katika maeneo yao.

Hata hivyo amesema kuwepo ushirikiano baina ya Waalimu na serikali za wanafunzi itapelekea wanafunzi kuweza kufuata sheria za skuli na kudumisha heshima kwa viongozi waliowachaguwa na jamii kwa ujumla.

Nae Mlezi wa Serikali ya Wanafunzi katika Skuli hiyo Mariam Haji Ramadhan ameitaka serekali hiyo kushirikiana na uwongozi wao ili kuweza kuongeza juhudi  za wanafunzi na kusoma kwa bidii jambo ambalo litawawezesha kufaulu vizuri mitihani yao ya Taifa.

Kwa upande wake Raisi mteule wa Serikali ya wanafunzi katika skuli hiyo nd.Najash Mbwana Zubeir ameahidi kutekeleza ahadi alizoziweka kwa vitendo kwa faida ya wanafunzi na skuli kwa ujumla.

Jumla ya wanafunzi 3 wameshiriki kugombea nafasi ya uraisi ambapo nd.Najash Mbwana Zubeir amechaguliwa kuwa Raisi kwa kupata kura 95,Asya Amir Said alipata kura 9 na Salma Rashid Salum alipata kura 2 kati ya kura 124 zilizopigwa na 18 zimeharibika.

                                        Takdir Ali.