WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imewaomba  wazazi kuwa na ukaribu mzuri na watoto wao pamoja na kufuatilia maendeleo ya masomo yao kwa kushirikiana na walimu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo,  Simai Mohamed Said, alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuwazawadia wanafunzi 50 waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne katika skuli za sekondari za Kijini na Matemwe Mbuyutende Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema iwapo wazazi watashirikiana na walimu katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi, kiwango cha elimu kitaendelea kuimarika hasa vijijini badala ya majukumu yote kuachiwa walimu.

Amesema serikali imeamua kuimarisha miundombinu katika sekta ya elimu ikiwemo kujenga skuli za ghorofa pamoja na kuondoa tatizo la upungufu wa madawati na kumpongeza Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuendelea kuimarisha elimu Zanzibar.

Aidha  ameupongeza mradi wa huduma za jamii wa Best of Zanzibar kwa kutoa masomo ya ziada ya kiingereza, hisabati na sayansi ambayo yamesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa Kijini na Matemwe Mbuyutende kila mwaka.

Meneja mradi wa huduma za jamii wa Best of Zanzibar, Aminata Keita, alisema mradi huo umegawika sehemu tatu; kutoa elimu ya afya na mazingira, kuinua kiwango cha ufaulu kwa kutoa masomo ya ziada pamoja na kampeni ya kuvisha watoto viatu kuanzia wenye umri wa miaka minne  mpaka minane katika skuli hizo.

Amesema viatu 400 vitatolewa kwa wanafunzi wa maandalizi na darasa la kwanza katika skuli ya Kijini na Matemwe Mbuyutende mwaka huu.

Kwa upande wake, Ofisa mradi wa Best of Zanzibar, Ali Suleiman Hamad, alisema mradi huo umeamua kuongeza walimu wa masomo ya ziada kutoka 10 mpaka 16 wa kufundisha masomo ya sayansi, hesabu na kingereza baada ya matunda kuanza kuonekana katika mradi huo.

Vijiji vya Kijini na Matemwe Mbuyutende vinakabiliwa na tatizo la umasikini kutokana na ardhi yake kuwa na mwamba wa mawe na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi na kuathiri mahitaji ya wanafunzi kama viatu na sare kabla ya kuanza kunufaika kupitia mradi huo.