w3anafunzi

Polisi nchini Burundi inawashikilia kundi kubwa la wanafunzi wa sekondari kwa kosa la kuharibu picha ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza.

Vijana hao wanakabiliwa na kosa la kumtukana kiongozi wa nchi, kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha miaka mpaka kumi jela. Wakazi mjini Bujumbura wanasema, watu wawili wamejeruhiwa siku ya Ijumaa pindi polisi walipopiga risasi kutawanya wanafunzi waliokuwa wakiandamana.

Waangalizi wanasema maafisa wa serikali walianza kupambana na kile kinachoonekana kuongezeka kwa visa vya kuharibu picha ya rais katika vitabu vya wanafunzi shuleni.

Makundi ya vijana yamehojiwa kutokana na matukio hayo na idadi kubwa inakabiliwa na mashtaka.

Mamia ya wanafunzi, wengine wakiwa na umri mdogo wa miaka kumi na miwili wamefanya maandamano kutokana na kamatakamata hiyo, lakini wanasema polisi wamefyatulia risasi.

Mwezi uliopita, zaidi ya wanafunzi mia tatu walitimuliwa shuleni katika mji wa Ruziba baada ya walimu kukuta vitabu vyenye picha ya rais vimeharibiwa kuandikwa ujumbe wa matusi.

Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikiwa masuala ya watoto UNICEF limelaani kukamatwa na kufukuzwa kwa watotot hao, na kusema shule zinatakiwa kuheshimiwa kama maeneo salama kwa watoto.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi nchini Burundi tangu rais Nkurunziza kuamua kuwania muhula wa tatu kinyume cha katiba ya nchi hiyo hapo mnamo mwaka jana.

Zaidi ya watu mia nne na hamsini wameuawa.