Wanajeshi Gabon wapindua Serikali ya Ali Bongo

Kundi la wanajeshi nchini Gabon limetangaza kwamba limetekeleza mapinduzi ya serikali katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kwamujibu wa taarifa kutoka BBC imeripoti kuwa Wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita wanashika doria katika barabara za mji mkuu Libreville.

Aidha Shirika la habari la AFP inasema milio ya risasi imesikika jijini humo.

Amri ya kutotoka nje imetangazwa.

Tangazo kutoka kwa kundi la vijana wa umri wa makamo linatangazwa na kurudiwa katika kituo cha redio cha serikali nchini humo, ambapo wanasema kumekuwepo na wasiwasi kuhusu uwezo wa Rais Ali Bongo kuongoza nchi hiyo.

Wanajeshi hao wamesema wamechukua hatua hiyo “kurejesha demokrasia” na wametangaza kwamba wanataka kuunda ‘Baraza la Taifa la Ufufuzi/Ukombozi’.

Wamekosoa hotuba ya Mwaka Mpya iliyotolewa na Rais Bongo mnamo 31 Desemba, na wanasema kwenye hotuba hiyo mawazo yake yalionekana kutotiririka na sauti yake ilikuwa dhaifu.

Ali Bongo amekuwa akipokea matibabu nchini Morocco
Ali Bongo amekuwa akipokea matibabu nchini Morocco

Bw Bongo amekuwa nje ya nchi hiyo kwa zaidi ya miezi miwili, akipokea matibabu nchini Morocco kutokana na maradhi ambayo hayajafichuliwa baada yake kuugua akiwa ziarani Saudi Arabia 24 Oktoba kuhudhuria mkutano mkubwa wa kiuchumi nchini humo.

Taarifa zinasema alikumbwa na kiharusi.

Familia ya Bongo imetawala taifa hilo kwa miaka 51 iliyopita, na imetuhumiwa kwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa kutokana na rasilimali za taifa hilo.

Rais Ali Bongo alichukua madaraka ya kuiuongoza nchi hiyo kutoka kwa baba yake Omar Bongo mwaka 2009, ambaye aliiiongoza nchi hiyo ya Afrika magharibi kwa zaidi ya miaka 40.

Alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2016, katika zoezi lililotawaliwa na ghasia na tuhuma za udanganyifu.

katika uchaguzi huo, Bw Bongo alipata ushindi kwa 49.8% ya kura naye Bw Jean Ping akapata 48.2 % ya kura, kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.

Kiongozi wa upinzani Jean Ping
Kiongozi wa upinzani Jean Ping

Bw Ping alisema uchaguzi huo ulijaa udanganyifu na “hakuna ajuaye” hasa nani alishinda.

Kabla ya kuingia katika siasa, Ping aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.