Wanajeshi walioandamana kwenda ofisi ya waziri mkuu Ethiopia wahukumiwa vifungo jela

Mahakama ya jeshi nchini Ethiopia imewahukumu wanajeshi 66 kati ya miaka 5 na 14 kwa kuandamana kwenda ikulu ya waziri mkuu Abiy Amhed mwezi Oktoba mwaka huu na kwa kuvunja kanuni za jeshi, kwa mujibu wa maafisa.

Wanajeshi hao 66 walikuwa miongoni mwa wanajeshi 200 waliokuwa wamevaa sare ambao walifika wakiwa wamejihami kwenye majengo ya ikulu ya Abiy tarehe 10 Oktoba katika kile serikali ilisema lilikuwa ni shinikizo na kutaka waongezewe mshahara.

Lakini Abiy ambaye alionyeshwa kwenye televisheni akifanya mazoezi na wanajeshi hao alisema viongozi wao walikuwa na nia ya kusitisha mabadiliko nchini humo na wanajeshi ambao hawakutajwa majina walisema walijutia kupoteza fursa ya kumuua Abiy.

Kanali Meshesha Areda, mkuu wa mahakama za kijeshi aliwaambia waandishi wa habari kuwa mahakama ya jeshi ilimhukumu mwanajeshi mmoja miaka 14 na wengine 65 kati ya miaka 5 na 13 kwa kukiuka kanuni za jeshi.

Hakujakuwa na taarifa kuhusu hatua za kijeshi walizochukuliwa wanajeshi wengine waliokuwa kwenye kundi hilo.

Wakili wa wanajeshi hao Desalegn Dana alisema atakata rufaa kwa washukiwa wachache.Tangu ateuliwe mwezi Aprili Abiy mwenye miaka 42 ameongoza mabadiliko kadhaa kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika ikiwemo kuwasamehe watoro waliokuwa wamepigwa marufuku na serikali za awali.S

Pia amekiri na kulaani udhalimu uliokuwa ukifanywa na vikosi vya usalama na hata kuwafananisha na magaidi.

Lakini ghasia zimekumba taifa hilo la watu milioni 100, na uhasama wa kikabila umekuwa changamoto kubwa.