Wananchi wa mkoa wa kaskazini Unguja wametakiwa kulitumia soko la wazi la kibiashara linalofunguliwa kila mwezi kwenye kijiji cha Nungwi ili kuweza kuuza na kununua biashara za asili zinazotengenezwa visiwani Zanzibar.

Akizungumza katika halfa ya ufunguzi wa soko hilo la kibiashara lililoandaliwa na tamwa  Mkurugenzi wa halmashauri ya kaskazini A Mussa Ali Makame amesema kufunguliwa kwa soko la kuuza na kununua bidhaa mbalimbali za asili litaweza kutoa fursa kwa wananchi wakiwemo wajasiriamali.

Hata hiyo wamewataka wafanya biashara kuweza kushajihika kuuza biashara wanazozalisha kwani kilio kikubwa kiupande wao kilikuwa ni upatikanaji wa soko la uhakika.

Mussa amesema  nungwi ni kijiji ambacho kipo mbele katika utalii hivyo soko hilo litaweza kuinuka kwani wageni wengine watashajihika kutembelea eneo hilo na wengi wao hupendelea kutumia bidhaa za asili zilizotengenezwa kwa miti ya asili na sio kemikali.

Hivyo amewataka wajasiriamali  wa mkoa huo kujitokeza katika kuuza biashara zao kwalengo la kuleta maendeleo na kujikwamua  katika hali  ngumu ya maisha.

Kwaupande wake Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar Dr Mzuri Issa wamesema tamwa itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wanawake ili kuona wanakwamuka na hali ngumu ya maisha na kuwacha utegemezi kwenye familia.

Amesema  wanawake endapo watazitumia taaluma wanazopewa na taasisi za kiraia wataweza kushajihika kwa kufanyakazi kwa bidii ikiwemo kujiekeza kwenye shughuli za ujasiriamali  kwani ndio mkombozi pekee kwa sasa.

Dr Mzur ametoa wito kwa wanaume wenye wake ambao wanaojishughulisha na kazi za ujasiriamali kuwaunga mkono wake zao  ili kuweza kufanikiwa zaidi na kupata maendeleo kwa pamoja.

Aidha amesema  mashirikiano ya pande mbili baina ya mke na mume endapo yatakuwepo yataweza kufanikisha kwa urasihi kazi za uzalishaji.

Nao baadhi ya wajasiriamali akiwemo Asha haji Issa na Hadija Bakari wamesema licha ya kuwa na muamko wa kufanya shughuli za ujasiriamali baada ya kupewa elimu lakini changamoto inayowasumbua ni kukosekana kwa malighafi za uhakika.

Wamesema upatikanaji wa malighafi kiupande wao umekuwa mgumu na bei haiyendi sambamba na kiwango cha mtaji wao hivyo wameiomba serikali iweze kuwasaidia ili kuweza kumudu gharama za manunuzi ili kuzalisha  bidhaa zenye ubora.

Aidha  wajasiriamali hao wametoa wito kwa  serikali  kuendelea kuwahamasisha wananchi kutumia bidhaa za asili ili kuweza kupatikana kwa soko la uhakika kupitia wanunuzi wa ndani.

Miongoni wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiamali wa ndani visiwan Zanzibar ni sabuni za mwani,shampuu,mikoba,vyetezo,liwa,vyakula vya mwani na mambo mengine.

Soko hilo lililofunguliwa Nungwa  na tamwa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mkokoton litakuwa wazi kila mwezi ili  kuwapatia soko la uhakika wajasiriamali wa kaskazini Unguja.s