Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Mjini Kichama Maulid Issa Khamis amewataka kinamama wa Umoja wa Wanawake (UWT) nchini kuwa na mashirikiano ili kuhakikisha wanakipatia ushindi mkubwa chama cha Mapinduzi katika uchaguzi ujao mwaka huu.

Katibu Maulid ameyasema hayo katika ukumbi wa CCM Tawi la Kwa wazee wakati alipokuwa akifungua Baraza la UWT Wilaya ya Amani, amesema wanawake wana nafasi na uwezo mkubwa wa kupeleka mbele maendeleo ya Chama na kuleta ushindi wa kishindo.

Amefahamisha iwapo akinamama watashirikiana na kuwaunga mkono wanawake wenzao wanaotarajia kuchukua fomu za uongozi wataweza kushinda na kushika nafasi za uongozi muda utakapofika.

Aidha ameeleza akinamama ndio wanaokuwa mstari wa mbele katika kukiletea ushindi Chama cha Mapinduzi kutokana na umoja walionao hivyo amewasisitiza kuimarisha umoja huo, amani na utulivu iliopo ndani ya chama .

“Kinamama ndio mnaokuwa katika mstari wa mbele katika kukiletea maendeleo chama cha Mapinduzi nakuombeni fursa msiziwache jitokezeni katika kuchukua nafasi za uongozi katika ngazi mbali mbali” alisema Mwenezi huyo.

Akitoa mada ya uhusiano wa viongozi na wanachama kuelekea uchaguzi mkuu wa wawakilishi, wabunge na madiwani Mwenezi huyo amewaasa wanajumuiya hao kuacha makundi na mifarakano katika jumuiya zao.

Amesema kuwa iwapo kutakuwa na makundi ndani ya jumuiya kutasababisha migogoro katika ustawi wa umoja huo na kupelekea vurugu na kuchagua kiongozi asiyekuwa sahihi.

Nae Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Amani Fatma Amran Abdullah amewataka akinamama kuchukua fomu za uongozi katika majimbo ili kukiendeleza chama kwani mwanamke ana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika chama cha Mapinduzi.

Amewasisitiza kinamama hao kuwa na ushirikiano pamoja na kuitumia vyema fursa hiyo adhimu ya kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za  uongozi kwa ngazi zote na kuweza kutoa maamuzi yaliyo sahihi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za UWT kipindi cha miezi Kaimu Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Amani Mwanamvua Mussa Chambo amesema hali ya kisiasa ndani ya Wilaya inaendelea vizuri na wanafanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja.

Kauli mbiu ya Baraza hilo ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na kujitokeza kuleta usawa wa kijinsia katika uchaguzi mkuu 2020/2025.