Serikali ya Nigeria imeripoti kuachiwa kwa wanafunzi waliotekwa na wapiganaji wa Kiislami kutoka mji wa Dapchi mwezi uliopita.

Wizara ya habari nchini Nigeria imesema wanafunzi 101 kati ya 110 walirudishwa mapema hii leo baada ya ‘juhudi za kichinichini za hapo awali.”

Jeshi ”lilisimamisha kwa muda” operesheni katika eneo hilo ili kuhakikisha ”maisha ya watoto hao hayamo hatarini,” taarifa hiyo imeendelea kusema.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikuzingatia idadi ya wasichana waliofariki na imesema hakuna kikombozi kilicholipwa kwa wapiganaji hao.

Taarifa hata hivyo zinadokeza kwamba wasichana takriban watano walifariki wakiwa mateka, na msichana mmoja ambaye ni Mkristo bado hajasalimishwa na anaendelea kushikiliwa mateka.

Baba wa msichana huyo amesema anaendelea kuzuiliwa na wanamgambo hao kwa sababu amekataa kuslimu. Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, amesema ana furaha kwamba mwanawe huyo hakuikana dini yake.

Waziri wa habari na tamaduni, Alhaji Lai Mohammed, amesema kwenye taarifa kwamba wasichana hao waliachiliwa ”katika hali isiyo ya kawaida” kutokana na “usaidizi wa marafiki wa nchi hii.”

“Serikali ilikuwa na uhakika kwamba vita na majibizano havingekuwa suluhu kwani ingehatarisha zaidi maisha ya wasichana hao, na mfumo wa kutotumia nguvu ndio uliokuwa umependekezwa,” Bw Mohammed aliongeza.

Pia alidokeza kwamba idadi hiyo huenda ikaongezeka kwa sababu wasichana hao hawakukabidhiwa kwa mtu binafsi , ili kutoa idadi rasmi ya wasichana hao.

Wasichana hao walichukuliwa katika shule hii ya mabweni Dapchi, jimbo la Yobe mwezi FebruariWasichana hao walichukuliwa katika shule hii ya mabweni Dapchi, jimbo la Yobe mwezi Februari

Mzazi Kundili Bukar aliambia BBC waasi hao wanaoaminika kuwa wa Boko Haram – waliingia katika mji huo kwa msafara wa magari mapema siku ya Jumatatu na kuwasalimisha wasichana hao kwa jamii.

Alisema wasichana hao walionekana kudhoofika na kuchoka – licha ya kwamba ripoti zinasema wasichana hao walipata nguvu ya kukimbia na kurudi nyumbani baada ya kuachiliwa huru.

Mzazi mwengine, Manuga Lawal, amesema aliweza kuzungumza na mwanawe ambaye alikuwa miongoni mwa waliotekwa kwa njia ya simu.

Mmoja wa wasichana walioachiliwa, akizungumza kwa simu na mmoja wa jamaa zake, amesema wasichana watano walikanyagwa na kufariki walipokuwa wanalazimishwa kuingia kwenye magari na kuondoshwa wakati wa kutekwa.

Msichana huyo amesema walipelekwa msituni hadi kwenye eneo lililokuwa limezungushwa ua. Alipoulizwa iwapo walikuwa wanalishwa vyema, amesema walilazimika kujipikia chakula chao.

Serikali bado haijazungumzia vifo vya wasichana hao.