WANAFUNZI wa kike visiwani Zanzibar, wamehimizwa kuyatumia kwa vitendo  maneno “Hapana Kudhalilisha” na sio kwa maneno matupu yasiyoonesha kuwa wanachukia kwelikweli ndani ya nyoyo zao.

Akizungumza katika kongamano la kuadhimisha ‘Siku ya Mtoto wa Kike Duniani’ lililofanyika skuli ya sekondari Ben Bellah juzi, Mkurugenzi wa Idara ya Wanawake na Watoto Nasima Haji Chum, alisema kufanya hivyo kutawezesha vita dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kupata mafanikio.

Katika kongamano hilo lililowashirikisha wanafunzi wa skuli za sekondari Forodhani na Ben Bellah likilenga kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike, Nasima alisema watoto wa kike wanakumbana na changamoto nyingi za  kudhalilishwa kimwili na kijinsia.

Alisema vitendo hivyo ni hatari kwao kwani vinaweza kuwaharibu kisaikolojia na kuwafanya waishi kwenye mazingira magumu.

Aidha alisema kuwa watoto wa kike wanakumbana na changamoto nyingi za  kudhalilishwa ikiwemo kimwili kijinsia jambo ambalo linaweza kuwaharibu kisaikolojia katika maisha yao.

Mkurugenzi huyo aliwataka wasichana wajitambue na wasikubali kukaa kimya wanapofanyiwa vitendo hivyo bali wawakabili wazazi, kwani kunyamaza kutaonesha hawajitambui na pia kunaweza kuwasababishia maradhi yasiyoyatarajia.

Alisema katika hali ya kawaida, hakuna mzazi anayefurahia kuona au kusikia mtoto wake amefanyiwa uovu kwa kudhalilishwa, kwa hivyo amewasisitiza wasione aibu kuwa wawazi ili kuwezesha kutafutwa kwa ufumbuzi wa vitendo hivyo.

Bi. Nasima pia amewataka wanafunzi wasibaguane katika kutafuta elimu, bali washirikiane na kila mmoja aumwe pale mwenzake anapopata matatizo ikiwemo kufanya vibaya kwenye mitihani au kukumbwa na vitendo vya kudhalilishwa.

Kwa upande wake, Ofisa Watoto katika Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Mohammed Jabir Makame, alisema  elimu ya afya ya uzazi ni muhimu kwani inamuwezesha mtoto  kupata makuzi yaliyo bora.

Katika kongamano hilo  wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Forodhani  wamesema kuwa elimu ya Afya ya Uzazi itolewe kabla ya kukua kwani afya ya uzazi kunamsaidia mtoto kuweza kukua kiakili na kuweza kujitambua katika maisha yake.

Wanafunzi walioshiriki kongamano hilo, wameomba  kuanzishwa utaratibu wa kuwapa watoto wa kike elimu ya afya tangu wakiwa skuli ili kuwafanya wasijiingize katika vitendo vinavyoweza kuwaharibia malengo yao ya maisha.

Mada kuu katika kongamano hilo ilikuwa, “Afya ya uzazi itolewe kabla au baada ya kukua ili kukuza usawa wa kijinsia.”