Wanafunzi katika Skuli za sekondari wametakiwa kuishajihisha jamii na kujiweka tayari katika masuala ya uzazi na unyonyeshaji salama wa ziwa la mama.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa wa afya kitengo cha lishe ndugu Omar Saleh Machano wakati wa mdahalo juu ya unyonyeshaji wa ziwa la mama kuwa msingi wa maisha uliofanyika huko Skuli ya Bambi na kuwashirikisha wanafunzi wa skuli ya Mpapa na Bambi sekondari.

Amesema kwa vile wanafunzi wa sekondari baada ya miaka michache huingia katika ndoa hivyo ni muhimu kuelewa taaluma ya unyonyeshaji kwa jinsia zote ili kupata vizazi vyenye afya bora.

Nae Afisa wa elimu ya watu wazima wilaya ya kati Maalim Issa Suleiman ameziagiza taasisi mbali mbali kuendeleza midahalo kwa wanafunzi ili kuwa na upeo wa kujieleza na kufahamu pamoja na kukuza kipaji juu ya mada zinazojadiliwa.

Mdahalo huo ulioandaliwa na wizara ya afya kitengo cha lishe umezungumzia umuhimu wa unyonyeshaji wa ziwa la mama muhimu kwa mtoto ambapo skuli ya Bambi sekondari iliyokataa hoja hiyo iliibuka kuwa mshindi wa mdahalo huo kwa point 78.63 na Mpapa sekondari kupata point 71.62.