Watanzania wanne waelekea kwenye mashindano ya kuogelea Nchini China

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Kuogelea nchini (TSA), Asmah Hilal amesema timu ya wanamichezo wanne imeondoka nchini kuelekea China usiku wa Disemba 7, na  imeambatana na kocha Alexander Mwaipasi na Mwenyekiti wa chama chao, Imani Dominick.

Mashindano ya dunia ya kuogelea yanatarajiwa kufanyika nchini China kuanzia Desemba 11 mpaka 16 huko ‘Hangzhou Olympic and International Expo Center’

Waogeleaji ambao wamekwenda kwenye mashindano hayo ni Kalya Temba na Celina Itatiro kwa upande wa wanawake na Collins Saliboko na Hilal Hilal kwa upande wa wanaume.

Akiongelea maandalizi yao Asmah amesema, “Ni matarajio yetu kuwa watafanya vizuri pamoja na changamoto mbalimbali tunazokabiliana nazo, mashindano yatakuwa magumu kwani waogeleaji nyota wa Dunia nao watakuwepo”.

Mashindano haya ni ya 14 ambapo yatafanyika kwenye bwawa la kisasa la kuogelea lenye urefu wa mita 25. Pia Bwawa hilo linahamishika na kwasasa lipo kwenye uwanja wa mchezo wa Tenisi lakini katika mashindano haya litaondolewa na kuwekwa eneo la wazi zaidi.