Jumla ya watoto 12 pamoja na kocha wao wa Mpira wa Miguu ambao walipotelea pangoni tangu Juni 23 wameonekana wakiwa hai katika moja ya pango lililojaa maji Jimbo la Chiang Rai nchini Thailand.

Watoto hao wakiwa ndani ya pango ambapo wamekutwa na waokoaji

 

Vijana hao wenye umri wa kati ya miaka 11 hadi 16 pamoja na kocha wao mwenye umri wa miaka 25  wameonekana mita 400 kutoka eneo ambalo walikuwa wakicheza baada ya kuingia katika pango moja wakati likiwa kavu na ghafla baada ya muda mvua kubwa ikanyesha na kuwazuia kutoka katika pango hilo.

Kikosi cha waokoaji wa vijana hao kimeeleza kuwa kiwango cha maji katika pango hilo ni kikubwa kiasi cha kuleta ugumu wa kuwatoa vijana hao kwa haraka zaidi lakini juhudi kubwa zinafanyika kuweza kufanikisha uokoaji kwa haraka iwezekanavyo .

Watoto hao wakiwa katika picha kabla ya kuingia katika pango
hilo

Vijana hao waligunduliwa na kikosi cha uokoaji cha Uingereza usiku wa Jumatatu baada ya kuombwa kwenda kusaidia harakati hizo japo juhudi za kuwaokoa kwa haraka zimeshindikana baada ya njia ya kuyanyonya maji katika pango hilo kushindikana na endapo waokoaji wataamua kusubiri maji yakauke basi vijana hao watakaa kwa muda wa mwezi mmoja katika pango hilo.

Kwa mujibu wa jeshi la nchi hiyo, njia pekee inayoweza kuwanusuru vijana hao kwa haraka zaidi ni kujifunza namna ya kuogelea ili waweze kutoka au wasubirie mwezi mmoja upite ili maji yapungue katika pango hilo.

Bonde hilo la Tham Luang limekuwa na historia ya kujaa maji kipindi cha mvua ambapo mvua hizo huwa zinanyesha hadi miezi ya Septemba na Oktoba.