Zaidi ya wananchi 82 katika tarafa ya Nguruka Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wanaofanya shughuli za uvuvi katika ziwa Nyamagoma wameliwa na mamba huku watu 25 wakijeruhiwa na wengine kuachwa na vilema vya maisha.

Hayo yalielezwa na wananchi hao wakipokea boti 10 za kuvulia samaki zilizotolewa na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (ENABLE) linalojishughulisha kujengwa uwezo wa kiuchumi kwa wananchi wa mkoa Kigoma kwa kuanzisha miradi ya utunzaji mazingira na miradi ya kuongeza kipato.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chagu, Lameck Martin akitoa taarifa kwa ujumbe wa viongozi wa taasisi hiyo ulioongozwa na Mwakilishi Mkazi wa ENABLE nchini, Tom Smis alisema kuwa mamba wamekuwa na athari kubwa kwa watu wanaofanya shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ambayo vifo hivyo vimetokea wamekuwa wakihangaika kutafuta njia za kukabiliana na hali hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa kimesababishwa na zana duni za uvuvi wanazotumia, ikiwemo mitumbwi ambayo imekuwa ikipinduliwa na mamba na wengi wao kuliwa au kuathiriwa vibaya.

Akieleza boti za mbao walizokabidhiwa na uongozi wa ENABLE zitasaidia kukabiliana na hali hiyo kwani wanaamini zimefanyiwa utafiti kusaidia kukabiliana na tishio la mamba ukilinganisha na mitumbwi waliyokuwa wakitumia.

Akikabidhi mitumbwi hiyo kwa wananchi hao Meneja mradi wa mradi huo, Cheyo Mayuma alisema kuwa ENABLE imetoa msaada huo wa boti 10 za mbao ikiwa ni sehemu ya jumla ya boti 25 zilizopangwa kutolewa kwenye vijiji vya Chagu, Mtego wa Noti na Kasisi ambazo zimekuwa vikiathirika zaidi na mamba na hasa kutokana na mitumbwi ya kiasili inayotengenezwa na miti waliyokuwa wakitumia.

Ofisa Maliasili na Mazingira Wilaya ya Uvinza, Kechegwa Masumbuko alisema kuwa boti hizo zimetengenezwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na mamlaka ya usimamizi wa usalama wa nchi kavu na majini