MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘B‘  Rajab Ali Rajab, amesema vita  dhidi ya uvuvi  haramu inaweza  kufanikiwa  iwapo  vyombo vya sheria  vitakuwa tayari  kushirikiana  na kikosi cha KMKM  pamoja na kamati za uvuvi kwa kuhakikisha hukumu inatolewa kwa wahusika pindi wanapofikishwa katika vyombo vya sheria.

Alisema  iwapo wahusika wa vitendo hivyo wataonewa muhali pindi wanapokamatwa na kufikishwa  katika vyombo vya sheria  bila ya kuchukuliwa hatua  stahiki dhidi yao, vitendo hivyo vitaendelea kujitokeza na kuathiri  uchumi wa taifa kupitia viumbe vya bahari.

Kauli hiyo ameitowa katika fukwe ya Kiwengwa mara baada ya kupokea taarifa kutoka  Kikosi cha KMKM kilichokuwa kinafanya doria ya kawaida na kufanikiwa kukamata wavuvi ambao walikuwa  wanatumia vifaa  visivyokuwa sahihi.

Alisema  uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na kikosi hicho utahakikisha sheria zinachukuliwa kwa wale wote waliokamatwa na kuhusika na shughuli za uvuvi haramu ili iwe fundisho kwa wavuvi wengine ambao wanaenda kinyume na sheria za uvuvi zilizowekwa na serikali.

Aidha,  Mkuu huyo wa Wilaya amemuagiza Sheha wa Shehiya ya Kiwengwa, pamoja na Afisa uvuvi wa Wilaya kuiangalia kwa kina sheria ya uvuvi  juu ya watu wanaoanzisha kambi kwa ajili ya uvuvi, ili kujua muda sahihi wanaotakiwa kuweka  kambi  pamoja na muda wa kumalizika kambi  hiyo   ili  kuzuia vitendo hivyo visiendelee kujitokeza.