Wavuvi wanane wamedaiwa kupatikana hai kwenye Bahari Hindi siku 18 baada ya mashua yao kuzama walipokuwa wakivua samaki. Mashua yao ilizama Disemba 8, 2019 katika eneo la Ziwayu, kaunti ya Kilifi na wamekuwa wakisakwa huku wengi wakiamini waliangamia.

wavuvi hao walipatikana lakini wako katika hali mbaya na wanapewa matibabu ya dharura katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.

Katika kile kinasikika kama tukio la kwenye sinema, wavuvi hao walipatikana mbali na mashua yao ilipozama na kundi la wavuvi wengine. Ripoti hiyo imedai kuwa, walikuwa kwenye mashua ya Alhafidh Fibre 15HP ambayo ilipigwa na mawimbi makali na hivyo kuzama.

Baada ya mawimbi kuwashinda kudhibiti mashua yao wavuvi hao waliamua kuruka majini ili kujiokoa. Imeelezwa kuwa, walipokuwa majini wakijaribu njia za kujitoa, walikula samaki waliokuwa wamevua kabla ya tukio hilo la ajabu.