Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi.Mary Maganga ametoa wiki moja kwa makampuni yanayozalisha bidhaa zinazofungasha chupa za plastiki kuandaa mikakati inayotekelezeka itakayoonesha udhibiti wa chupa za plastiki wanazozizalisha na kuiwasilisha Ofisi ya Makamu wa Rais April 20, 2021.

Bi. Mary Maganga ametoa agizo hilo leo katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha wadau wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji wa bidhaa zinazofungashwa kwa chupa za plastiki za rangi na kusema kuwa uchafuzi wa mazingira utakanao na chupa za plastiki zenye rangi umekuwa changamoto nchini. 

“Kutokana na umuhimu wa udhibiti wa taka za plastiki tunao wajibu wa kuungana pamoja ili kuwa na juhudi za pamoja katika kukabiliana na changamoto za udhibiti wa taka zitokanazo na plastiki kama Kanuni ya 4 ya Kanuni za Usimamizi wa taka ngumu za mwaka 2009 chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 zinavyoelekeza,” amesema Bi. Mary.

Aidha, Bi Maganga alifafanua licha ya jitihada za kuziondosha chupa hizo katika mazingira bado kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa makampuni ya kutosha yanayojishughulisha na urejelezaji wa chupa hizo hivyo chupa hizo zimeendelea kuzagaa katika mazingira ya watu na kuchangia uchafuzi wa mazingira.

“Natoa wito kwa jamii kukabiliana na changamoto za udhibiti wa taka zitokanazo na plastiki ambapo mzalishaji ana wajibu wa kuondosha kwenye mazingira taka zitokanazo na bidhaa anazozalisha,” alisisitiza Maganga.

Kikao hicho kimeshirikisha wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mwakilishi kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) na wawakilishi wa wamiliki wa viwanda nchini.