Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Sadala maarufu ‘Mabodi’,amewataka viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF ) kutotumia mipasuko na migogoro yao kuhatarisha amani na kwamba Wazanzibari kwa ujumla hawapo tayari kuingia katika machafuko ya kisiasa kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache.

Aliyasema hayo jana katika hafla ya kukabidhi basi lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Magomeni mjini Unguja,  Jamal Kassim Ali kwa chama hicho, alisema CCM itaendelea kusimama imara na kupaza sauti inapoona baadhi ya watu wachache wanavunja sheria za nchi kwa makusudi bila ya kujali misingi ya utu na haki za binadamu.

Alisema baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi kujiunga na ACT-Wazalendo wameshuhudia vitendo vya uvunjifu wa sheria kwa makusudi vinavyofanywa na wanachama wa ACT Wazalendo.

Katika maelezo yake, Mabodi aliongeza kuwa wanachama wa ATC-Wazalendo wamefanya uharibifu wa mali za CUF ikiwemo kuchoma nguo za chama hicho, bendera, kung’oa samani zilizoko katika ofisi mbalimbali sambamba na kutumia dini katika harakati za chama hicho.

“Mambo yote hayo ni ishara za wazi zinazochochea vurugu na migogoro baina ya wanachama wa vyama hivyo viwili, zinazoweza kuingiza nchi katika athari kubwa ya machafuko”