Wazazi na walezi wenye Watoto wenye ulemavu kuwashirikisha katika harakati za kijamii

Wazazi na walezi wanaoishi na watoto wenye ulemavu wa akili wametakiwa kuwashirikisha watoto wao katika harakati za kijamii ikiwemo kuwapeleka skuli ili waweze kunufaika na haki zao za msingi.

Akizungumza na Zanzibar24 nje ya Mafunzo ya Umuhimu wa kuwapeleka watoto wenye ulemavu wa akili skuli mwakilishi kutoka Taasisi ya kutoa huduma za jamii (Alliance Club) Khadija Muhammed amesema licha ya kuelimishwa kuwapeleka watoto Skuli lakini baadhi ya wazazi hawapeleki watoto wao skuli.

Amesema wakati umefika kwa kila mzazi kujua wajibu wake juu ya kusimamia haki za maelezi ya watoto katika familia zao ili watoto wenye ulemvu waweze kunufaika na fursa na kupata elimu.

Amesema watoto wenye ulemavu wa akili ni watoto wenye uwezo mkubwa katika kujifunza kinadharia na kwa vitendo wakiwa madarasani jambo ambalo linajenga uhusiano mzuri kati yao na wanafunzi wengine.

Akiwasilisha mada juu ya kuwaepusha watoto wenye ulemavu wa akili na hatari za kiafya, Mkufunzi wa Chama cha Msalaba Mwekundu (Red cross) Zanzibar Rashid Ali Hassan amesema ni vyema kwa wazazi kuhakikisha wanafatilia nyendo za watoto wao wakati wanapocheza na watoto wenzao.

Amesema tathmini inaonesha kuwa familia nyingi hazifatilia watoto walio na matatizo ya akili jambo ambalo ni kinyume na taratibu za haki za binaadamu.

Aidha ametowa wito kwa wazazi, walezi na walimu wanaosimamia watoto hao kujifunza namna ya kuwasaidia watoto hao wanakutwa na ajali mbalimbali nyumbani ikiwemo kuvunjika viungo na kujikata.

Wakati huo huo Mwalimu mkuu wa kitengo cha Watoto wenye Ulemavu wa akili katika Skuli ya Jang’ombe Msingi A Mwanakombo Khamis Rashid amesema watoto wenye ulemavu wa akili wamekuwa wanahamasa kubwa ya kujifunza wakiwa madarasani.

Amesema katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu kwa wakati ni vema kwa wizara ya elimu kuwaandaa mitaala maalumu ili kuwawezesha watoto hao kujifunza kwa wepesi pamoja na kuwapatia vifaa vya kuwafundishia.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Chama cha michezo kwa Watu wenye Ulemavu wa akili Zanzibar (Special Olimpic), Chama cha Msalaba mwekundu (Red cross) pamoja na Taasisi inayotowa huduma kwa jamii (Alliance Club) kwa lengo la kuwapa wazazi elimu ya afya kwa watoto wenye ulemavu wa akili.

Na.Fat-hiya Shehe Zanzibar24