Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitano katika Kijiji cha Kibigoji kata ya Kibati Turiani Wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro mbali na kuzaliwa akiwa na utata wa jinsi yake, pia amebainika kuwa na tundu kwenye kitovu ambayo tundu hiyo anapokunywa maji yanatoka.

Mama wa mtoto huyo, Mwajuma Athumani (31) alisema, alijifungua mtoto huyo Mei 18, mwaka jana, ndipo walipogundua mtoto huyo jinsia yake haieleweki hata hivyo hana uwezo wa kumpeleka kwenye hospitali kubwa kutibiwa.

Mwajuma alisema alipokua mjamzito hakuwa na tatizo lolote, alifanya shughuli zake za kilimo kama kawaida kwani tayari alikua ni mama wa watoto wengine wanne hivyo alipopata uchungu, ndugu zake walimpeleka hospitali lakini akiwa njiani alijifungua na kurudishwa nyumbani.

Baada ya wiki moja ndio tulienda hospitali nikawaonesha mtoto wakasema atapata chanjo, lakini hawakutupa kadi yoyote, na pia hawakuniambia jambo lolote kuhusu maumbile ya mtoto huyu”alisema

Alisema mtoto alianza kumsumbua kwa kuumwa mara kwa mara pia alikuwa na tundu chini ya kitovu, alimpeleka hospitali wanamchoma sindano na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Alisema kilichokua kikimsumbua ni kuvimba sana kwenye korodani ambapo alilazwa katika kituo kimoja cha afya kilichopo kijijini kwao na kutundikiwa dripu, lakini maji yalikua yakitoka kwenye tundu aliyokuwa nayo chini ya kitovu hadi ikabidi daktari atoe dripu na kumchoma sindano tu.

“Tuliondolewa hospitali wakatuambia tukaombe kibali kwa mkuu wa Wilaya tuweze kuchangisha fedha tupate bima ya matibabu na kumpeleka mtoto Muhimbili akapate matibabu.

Hapa alipo hatujui mtoto ni mwanamke au mwanaume, na tatizo linalomsumbua kibofu chametoboka ndani na pia koridani kuvimba zinamsumbua sana, hadi sasa mkojo unatoka tu hauwezi kukoma”.

Baba wa mtoto huyo, Nasibu Mussa (34) alisema alipopata taarifa kuwa mke wake kajifungua alishukuru ingawa alielezwa kuwa alijifungulia njiani akipelekwa hospitali Alisema alielezwa na mama mkwe wake kuwa mwaka huu wamepata matatizo, alimfunulia mtoto na kuona maumbile ya mtoto aliamua kumpeleka hospitali wapate ushauri.

Chanzo Habari leo.