Wanandoa, Amina Juma na Kanuno Tano wamejiua baada ya kuuguza mtoto wao kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Adam Kalonga ambaye ni babu wa Amina, mtoto Chiku Kudona (miezi 9) amekuwa akiugua muda mrefu na kichwa chake kuongezeka ukubwa.

Kalonga alisema Amina alikatisha uhai wake kwa kunywa vidonge mchanganyiko vinavyotibu magonjwa ya binadamu.

Alisema Tano, ambaye ni mume wa Amina naye aliamua kujiua kwa kujinyonga mbali kidogo na nyumbani kwao baada ya mkewe kujiua.

Matukio hayo yote mawili ambayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley aliyazungumzia katika mkutano wake na wanahabari alisema yalifuatana.

“Mmoja wa watoto wa familia hiyo ameugua ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu. Baada ya kumuuguza mtoto kwa muda mrefu mama aliamua kujiua,” alisema Nley.

Alisema baada ya taarifa za kifo cha mkewe kujulikana na mwili kuchukuliwa na polisi kwa uchunguzi, mumewe aliamua kujiua kwa kujinyonga akitumia pazia.

Kamanda Nley alisema matukio hayo mawili yameacha simanzi kwa familia, ndugu na majirani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na wanandoa hao katika shughuli mbalimbali za kijamii.