Mkurugenzi Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla ameishauri jamii kuchukua jitihada zaidi kwa watoto wao kuhakikisha wanapata huduma ya chanjo kwa ukamilifu.

Amesema tathmini inaonyesha kuwa baadhi ya wazazi na walezi hawakamilishi chanjo kwa watoto wao bila ya kujua kuwa kitendo hicho kinaweza kudhoofisha afya zao.

Dkt. Fadhil alitoa ushauri huo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari kutoka vyombo vya Zanzibar katika ukumbi wa Kitengo cha Huduma ya Mama na Mtoto (IRCH) Kidongochekundu.

Alisema mkakati wa huduma za chanjo umesaidia sana katika kuimarisha afya za watoto na kupunguza ama kuondosha kabisa baadhi ya maradhi yanayowasumbua.

Aliongeza kuwa mzazi anapompatia mtoto wake chanjo kamili anapunguza gharama ya matibabu na hupata nafasi ya kufanya shughuli za maenmdeleo kwa vile baadhi ya maradhi hayawezi kumsumbua .

Alikumbusha chanjo kwa Zanzibar inatolewa bure kinyume na nchi nyengine ambazo huduma hiyo hutolewa kwa malipo hivyo amewataka wananchi kuitumia fursa hiyo inayotolewa na Serikali na wafadhili ili kuwalinda watoto na maradhi yanayotibika kwa njia hiyo.

Na Ramadhani Ali – Maelezo  Zanzibar.