Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewabana askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani wanaowabambikia madereva makosa yanayotokana na picha za mwendokasi zisizo na uhalisia na kushinikiza kupewa rushwa, kuwa watakaobainika kuanzia sasa watazilipa faini hizo wao na kuondolewa katika kitengo hicho.

Alitoa agizo hilo mjini Morogoro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maafikiano kati ya serikali na vyama vya watoa huduma za usafirishaji nchini juu ya kusitisha kusudio la madereva wa mabasi ya mikoani kufanya mgomo wakishinikiza kutimiziwa madai mbalimbali ikiwemo ya mikataba ya kazi.

Waziri Lugola alisema maamuzi hayo yametokana na makubaliano ya pamoja baina ya viongozi wa vyama hivyo vya usafirishaji na wizara mtambuka za serikali yaliyofanywa kwa nia ya kutatua changamoto walizowasilisha katika kikao hicho kuhusu kubambikizwa makosa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Alisema moja ya makosa yanayolalamikiwa na madereva hao ni pamoja tochi zinazopiga picha mabasi na kurushwa kwenye simu za askari ambazo zinakosa uhalisia wa tukio, ikiwemo kutoonekana namba za usajili na vibao vya alama za barabarani na kusababisha utata na mivutano yenye nia ya kujenga mazingira ya rushwa.

Waziri Lugola alisema kuanzia sasa askari wa usalama barabarani wanapaswa kupiga picha za makatazo mbalimbali ya barabara kwa mbele ya gari na picha zioneshe muonekano usio na mashaka wa gari, namba ya usajili na eneo la alama iliyokiukwa na dereva.

Alisema lengo ni kuwepo na ushahidi halali wa tukio husika na vinginevyo dereva mwenye kubakiziwa makosa hayo asichukuliwe hatua yoyote.

Pia alionya tabia ya baadhi ya askari kukamata mabasi yenye abiria na kuyafikisha Kituo cha Polisi kwa nia ya kumuadhibu dereva aliyetenda makosa na kuagiza jambo hilo liachwe mara moja na badala yake dereva aliyetenda kosa anapaswa kukamatwa katika kituo cha mwisho cha safari yake.