Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kangi Lugola amesema kuwa wapenzi wa jinsia moja hawapo hatarini hata kidogo Tanzania.

Lugola amesema japo ushoga ni kosa la jinai nchini Tanzania, wanaojihusha na vitendo hivyo hawatishiwi maisha na wala hawaikimbii nchi.

Akizungumza na gazeti la serikali la Habari Leo, Lugola amekanusha kuwa wapenzi wa jinsia moja wapo hatarini.

“Ninachosema ni kuwa Tanzania ni salama na hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kuwa sio salama bila ya kuwa na vigezo husika, kama mtu yeyyote anahatarishiwa maisha yake, basi napaswa kwenda polisi na mimi sijapata taarifa zozote kutoka polisi zinazoeleza kuwapo kwa mazingira hatarishi ya watu hao,” Lugola amenukuliwa akisema.

Serikali ya Tanzania imejitenga na kampeni ya Paul Makonda dhidi ya ushoga

Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alitangaza kuanza kampeni dhidi ya ushoga kwa kuunda kamati ya watu 17.

Makonda alisema haki za mashoga hazitambuliki kama haki za binaadamu nchini Tanzania na kuzitaka nchi zinazotetea vitendo hivyo kuwachukua mashoga wa Tanzania.

Baada ya kauli hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania ilitoa taarifa kuwa huo si msimamo wa serkali bali mawazo ya Makonda pekee.

Taarifa hiyo ilisema Tanzania itaendelea kuheshimu haki zote za binaadamu kama inavyotakikana na katiba ya nchi pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeisaini na kuiidhinisha.