Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesisitiza kwamba Serikali itaenzi na kuendeleza jitihada, maono na juhudi za aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli hususan katika ulinzi wa rasilimali za Taifa pamoja na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 13, 2021) wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

Mhe. Majaliwa ametaja mambo yatakayoendelezwa ni pamoja na  nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kuenzi lugha ya Kiswahili, kuunganisha na kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa Kitaifa.

“Serikali itaendelea kuimarisha huduma za jamii zikiwemo afya, elimu na maji pamoja na utekelezaji wa miradi inayoendelea na uanzishwaji wa miradi mipya. Pia itaimarisha makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuendeleza rasilimali fedha katika miradi ya kimkakati na kielelezo.”

Amesema Serikali itatekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira. “Kwa kasi tuliyoanza nayo, Serikali itaendelea kuongeza nguvu zake na hatimaye kukamilisha miradi hiyo.”
 
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh.116,784,244,000.00 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake kwa matumizi ya mwaka 2021/2022. Amesema kati ya fedha hizo, sh. 93,303,370,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 23,480,874,000.00 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.