Waziri mkuu Kassim Majaliwa, ameishukuru serikali ya Finland kwa jitihada ambazo nchi hiyo inazifanya kuisadia Tanzania kuondokana na umasikini ambapo amesema kuwa bado nchi ina fursa za uwekezaji na kwamba Serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki na bora kwa uwekezaji.

Ametoa kauli hiyo, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma alipokutana na Balozi wa Finland hapa nchini
Pekka Hukka anayemaliza muda wake ambapo amesema kuwa Sekta ambazo makampuni ya Finland inaweza kuwekeza hapa nchini ni pamoja na TEHAMA, nishati, usafiri, uchakataji wa mazao ya kilimo na misitu.

“Tunaishukuru Serikali ya Finland kwa misaada ambayo imeendelea kuitoa kama njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuondoa umaskini pamoja na kuongeza makusanyo ya mapato ili kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema.

Aidha amemtakia heri Balozi Hukka ambaye anatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa mwezi huu kwenda Tunisia ambako ndiko kutakuwa na kituo chake kipya cha kazi.

Kwa upande wake, Balozi Hukka amesema ataondoka Tanzania akiwa na kumbukumbu nzuri ambazo atazienzi na anataraji kukutana na Watanzania wengine ili aendelee kukuza mahusiano yaliyokuwepo.