Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa makao ya watoto wasiofuata taratibu za usajili wa watoto, wanaowatumia watoto kama mitaji au kwa maslahi binafsi na wanaoendesha makao hayo kwa minajili ya kidini na kikabila.

Amewataka pia wamiliki hao waache mara moja kuwalea watoto hao katika maadili yasiyofaa na yasiyo ya Kitanzania na kwamba maofisa ustawi wa jamii wahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha kuwa ni watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao ndiyo wanasajiliwa.


Alikuwa akizungumza jana usiku (Jumapili, Mei 26, 2019) kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam alikokuwa mgeni wa heshima wakati wa futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini humo.

“Nitoe rai kwamba watu mmoja mmoja, taasisi na makao wazingatie baadhi ya taratibu za msingi za uendeshaji wa makao kama vile mtoto kukuzwa katika mazingira ya familia, kuzingatia misingi ya kitaifa badala ya misingi ya tamaduni za kigeni.


“Mtoto kukuzwa kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto; kuzingatia umuhimu wa kuwa na mwendelezo katika dini ya mtoto na utamuduni wake; kutotenganisha watoto na ndugu na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma stahiki, kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji; na kutunzwa na  kuendelezwa hadi kufikia kimo cha utimilifu wao,” alisema.

Mapema, akielezea azma ya kuandaa futari hiyo, Mkurugenzi wa Chocolate Princess na mwandaaji wa kipindi cha televisheni maarufu cha The Mboni Talk Show, Bi. Mboni Masimba alisema jumla ya watoto yatima 325 walikuwa wamealikwa kushiriki futari hiyo.


Watoto hao wanatoka vituo vya Ijango Zaida Orphanage Centre kilichopo Sinza, Alzama Orphanage Centre (Mbagala), Ashura Foundation (Vingunguti), Madina Orphanage Centre (Tandale), Hiyari Orphanage Centre (Mbagala) na Hisani Orphanage Centre (Mwasonga).

Futari hiyo iliandaliwa na Mboni Masimba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Asure Yetim Vafki, United Bank of Africa (UBA), Junaco, Mo Dewji Foundation, Lake Oil, ASAS, AZAM, Uncle K Catering, Zurii, Simply Special Decor na State Oil na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo Balozi wa Uturuki nchini, Bw. Ali Davutoğlu, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Issa Othman, masheikh, maimamu wa misikiti na viongozi wa taasisi zinazojihusisha na malezi ya watoto yatima