Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakatoe taarifa katika shirika.

Mwijage alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa kuwepo kwa makontena 100, yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila kukaguliwa na TBS.

“Nawataka wafanyabiashara wote waliochukua kontena hizo, wajisalimishe haraka TBS kabla ya kufika Jumanne ili wakaguliwe. Najua kuanzia kesho ni mapumziko, lakini TBS itaweka dawati la kuwasikiliza mpaka Jumatatu na ikifika Jumanne hatua zitachukuliwa kwa wahusika wote,” amesema Mwijage.

Alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.

Aidha, alisema kwa mawakala wa forodha wote, waliohusika kutoa kontena hizo wizara yake itawasiliana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ili kuona hatua za kuchukua kwa kuwa serikali haiwezi kukubali mchezo huo.