Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amewataka Vijana kujituma katika michezo na sanaa  ili kufikia lengo la Serikali kuifanya michezo na Sanaa  kuwa ni  sehemu ya ajira na njia ya kuliongezeza mapato Taifa.

Hayo ameyasema huko Bungi Mkoa wa  Kusini Unguja katika Maadhisho ya miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambapo kwa Jimbo hilo kulifanyika  Bonanza la michezo lililoshirikisha timu za mpira wa miguu, Nage, Sarakasi Muziki wa kizazi Kipya , Dansa na Ngoma za asili.

Amesema kufanyika kwa bonanza hilo la Michezo ni njia moja wapo ya kuwakutanisha vijana na wazee kukaa pamoja na kujadili changamoto zinazoikabili jamii inayowazunguka ikiwemo suala la udhalilishaji.

‘’ Si kwamba bonanza hili limetukutanisha kwa kuonyesha michezo bali pia tujadili changamoto zilizomo ndani ya jamii ikiwemo suala la udhalilishaji ambao unaonekana kuota mizizi hapa Zanzibar hivyo kila sehemu tunapokutana tunatakiwa kulizungumzia hili.’’ Alieleza Waziri Tabia.

Amewataka viongozi wa Jimbo la Tunguu kuliboresha bonanza lijalo kwa kuwatunuku zawadi washindi na kuwatia ari ya kuweza kushiriki ili kuendeleza na kukuza michezo na Sanaa kwa kujipatia ajira kutokana na fani hizo.

Waziri Tabia amefurahishwa na utekelezaji wa ahadi za Mbunge  wa Jimbo hilo na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyowataka kuwatumikia wananchi na kuwaondolea changamoto zao.

Nae Mbunge wa jimbo hilo Khalifa Salum Suleiman amesema atahakikisha michezo katika jimbo hilo inakuwa ajira kwa vijana kwa lengo la kuona wanajikita kwenye michezo na kuijitoa katika makundi yasiofaa.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Mungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha michezo nchini kwa kuwahamasisha vijana kujikita katika fani hiyo ili kuondokana na umasikini na kuongeza ajira.