Waziri Ummy kuwapambanisha RC Tabora na Mara
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema atawapambanisha mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri na mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima katika jitihada zao za kupambana na vitendo vya ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni kwa kuwa matukio hayo yanatokea zaidi katika mikoa yao.
Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 9, 2018 wakati akifungua mjadala wa kitaifa wa changamoto za mimba na ndoa za utotoni ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu(UNFPA).
Ummy amesema Mara na Tabora ni miongoni mwa mikoa yenye changamoto ya vitendo hivyo, kwamba anataka kuona uhodari wa Mwanri na Malima katika kupambana.
Amesema mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na Malima wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na vitendo hivyo kwenye mikoa wanayoingoza.
“Lakini kuna jembe linaitwa Mwanri yeye anasema atakayepokea mahali sukuma, na wale kina mama wanaofanya chikichiki… sukumia mbali,” amesema Mwalimu na kusababisha watu kuangua kicheko.
Siku za hivi karibuni Mwanri amejizolea umaarufu baada ya kusambaa kwa video katika mitandao ya kijamii zikimuonyesha akizungumzia matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii akitumia maneno ya ‘sukuma ndani’ na ‘fyekelea mbali’ ambayo yamekuwa maarufu kwa sasa.
“Kwa hiyo nitawashindanisha Malima na Mwanri tuone nani atapata tuzo mwakani. Mwanri yupo imara kupamba na vitendo hivi sambamba na Malima,” amesema.
Kwa upande wake Malima amesema chanzo cha vitendo hivyo ni mila, desturi na tamaduni na kwamba anayetaka kupambana na vitendo hivyo lazima akumbane na ugumu.